Imeelezwa kuwa ujio wa magari mapya ya Jetour nchini Tanzania kupitia ushirikiano kati ya Jetour Global na Africarriers Group ni hatua muhimu katika kuimarisha biashara, kuongeza chaguo kwa watumiaji na kuendeleza ajenda ya Serikali ya kukuza viwanda na uchumi wa kisasa unaotegemea sekta binafsi.
Akizungumza katika uzinduzi wa magari hayo, Dar es Salaam, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema kuja kwa magari hayo kunafungua ukurasa mpya wa fursa za kiuchumi.
Amesema uwekezaji huo utazalisha ajira mpya kwa vijana katika maeneo mbalimbali yakiwemo mauzo, huduma za kiufundi, ushauri wa huduma kwa wateja, teknolojia ya habari na mawasiliano pamoja na huduma nyingine nyingi zinazohusiana na sekta ndogo ya magari.
"Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji na biashara. Pia Serikali imefanya maboresho makubwa katika sera, sheria na mifumo ya utoaji huduma ili kuvutia uwekezaji wenye tija, kuongeza uzalishaji, kukuza biashara na kuimarisha ushindani wa uchumi wetu", amesema.
Kapinga amesema uzinduzi huo unaendana kikamilifu na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano pamoja na Ajenda ya Taifa ya Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda na Biashara. Unadhihirisha dhamira ya kukuza ushiriki wa sekta binafsi, kuongeza matumizi ya rasilimali za ndani, kuhamasisha uhamishaji wa teknolojia na kuzalisha ajira kwa Watanzania.
Adha Kapinga amesema, uwekezaji huo utachochea ajira zisizo za moja kwa moja katika sekta za usafirishaji, bima, matangazo, huduma za kifedha na minyororo ya ugavi wa ndani.
Amesema hiyo ni ishara ya namna sekta binafsi inavyoendelea kuwa injini muhimu ya ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi, pia mbali na ajira, Jetour inaleta maarifa mapya ya kiteknolojia, mafunzo ya kitaalamu na mifumo ya kisasa ya huduma za magari, itasaidia kuongeza ujuzi wa Watanzania, kuimarisha ushindani wa sekta yetu ya magari na kuinua viwango vya utoaji huduma kwa manufaa ya watumiaji.
Kwa upande wa Mkuu wa Idara ya Sheria wa Kampuni za Africarries, Ngasa Mboje, alisema kwa mara ya kwanza wameleta gari zinazoendana na soko na mahitaji ya Watanzania kwasababu ni gharama nafuu.
Mboje alisema magari ya Jetour yanauzwa kwa njia mbili cash na mkopo, kwasababu kuna baadhi ya Watanzania hawawezi kumudu gharama kwa mara kwanza, hivyo unaweza kununua kwa mkopo na kulipa kidogo kidogo, huku ukiendelea kulitumia gari lako.




