Katambi Asisitiza Maadili, Ndoa 130 Zafungwa Dar


Na MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amesema ndoa ni kiini cha msingi, nguzo imara na kiunganishi kati ya uwepo wa serikali na masuala yote ya amani na usalama.

Katambi alisema hayo, katika hafla ya kufungisha ndoa 130 zilizodhaminiwa na Taasisi ya Al Hikma, wilayani Temeke, Dar es Salaam, juzi.

“Nitumie fursa hii kutoa pongezi zangu za dhati kwenu Taasisi ya Alhikma katika zama za sasa, changamoto ya mmomonyoko wa maadili kwa asilimia kubwa inachochewa na ongezeko la mahusiano yasiyo halali, migogoro ya kifamilia na mambo mahususi yanayowakabili viana, ndoa kama hizi ni sehemu ya suluhisho”, alisema.

Katambi alisema ndoa halali ni sababu ya mahusiano na kizazi halali kinachojenga familia halali ambayo ndiyo msingi wa kwanza wa jamii imara yenye maadili.

Alisema familia ikisimama vizuri jamii itasimama vizuri, hivyo taifa nalo litastawi na kuimarika katika suala zima la usalama na amani.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Sheikh Nurudn Kishki, alisema hadi sasa vijana 500 wamewasaidia kuwalipia mahari na kuwaozesha ni sawa kuwapa ndoa vijana 1,000 ukichanganya na wake zao.

Alisema taasisi hiyo imegundua vijana wengi wako tayari kuoa, lakini wanashindwa kulipia mahari za pamoja, pia lengo la taasisi hiyo kudhamini ndoa hizo ni kupunguza mambo machafu katika jamii.

Kishk alisema ndoa hupelekea kulinda maadili mema katika jamii na taifa kwa ujumla, vijana wengi wanaoshinda mitaani ni ukosefu wa kulelewa na wazazi wote wawili.

"Wanaume wengi tunahodari wa kuzalisha wanawake na kisha kuwatelekeza, watoto wengi wanalelewa na mama zao, hivyo kuna baadhi wa kinamama wanashindwa kuwalea watoto zao na kupelekea mmonyoko wa maadili katika jamii", alisema.