IGUNGA - TABORA
MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Shabani Hemed kwa kushirikiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Selwa Hamid wamemkabidhi Mkandarasi, William Polas Mkataba wa kujenga jengo jipya la Halmashauri hiyo.
Aidha, Jengo hilo litagharimu sh. bilioni 4.497 huku halmashauri hiyo ikiwa imepokea sh. bilioni 1.0 kutoka serikali kuu inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza katika halfa ya utiaji saini mikataba iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo, Hemed amemshukuru Rais Dk. Samia kwa kuwaona Wananchi wa Igunga na kuridhia kiwango hicho cha fedha kitekeleze mradi huo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Selwa Hamid amesema serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia ni sikivu kwa sababu baada ya Halmashauri hiyo kupeleka maombi ikapatiwa fedha takribani sh. 4.497 bilioni kwa lengo la kujenga jengo hilo jipya.
Amesema wanaamini jengo hilo litajengwa kwa ubora na kasi inayotakiwa ikiwemo kuzingatia viwango stahiki.





