Tume ya Uchunguzi wa Matukio Yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, mwaka 2025 imeanza kusikiliza maoni ya wananchi wilayani Ilala , jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mjumbe wa tume hiyo, Balozi Ombeni Sefue, amewataka wananchi kujitokeza kutoa maoni yao kuhusu walicho shuhudia wakati na baada ya matukio yaliyotokea Oktoba 29, 2025.
Amesema hiyo ni fursa muhimu kwa wananchi na wasisubiri baada ya tume kumaliza kukusanya maoni ndipo waanze kulalamika.
“Tunataka kila mtu aliyeshuhudia ajitokeze katika tume. Isije akajitokeza mtu baada ya tume kumaliza kazi yake akaanza kulalamika. Tulipewa siku 90 na Rais (Dk. Samia Suluhu Hassan) ambazo zitamalizika Februari mwaka huu", amesema Balozi Sefue.
Ameeleza tume hiyo imezunguka katika mikoa mbalimbali nchini na hivi sasa inakusanya maoni katika ngazi za chini za wilaya ambapo aliwashukuru wananchi kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao.
“Katika Mkoa wa Dar es Salaam, tume imegawanyika. Wengine wako Temeke na wengine Ilala. Tutakuwa Kinondoni na Ubungo kisha Kigamboni", amesema Sefue.
Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewahimiza wananchi kujitokeza kutoa maoni yao mbele ya tume hiyo.
Amewataka walioathirika , kufiwa na nfugu zao, kujeruhiwa , kuharibiwa na kuibiwa mali zao kujitokeza.
Tume hiyo inayoongozwa na Jaji Othuman Chande, iliundwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kufanya uchungizi wa matukio yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 mwaka jana hapa nchini.

0 Comments