Mbeto: Jussa pilipili asoila inamuwashia nini


Na Mwandishi  Wetu, Zanzibar

Chama Cha Mapinduzi (CCM) imemtaka Makamu Mwenyekiti  wa ACT  Wazalendo Zanzibar, Ismail  Jussa  Ladhu, kujiandaa kisaikolojia kwani chama chake  hakitamudu kuhimili mikikimikiki ya CCM Oktoba mwaka huu.

Pia CCM imemtaka makamu huyo Mwenyekiti kuacha ngebe na mshawasha huku akiulizwa pilipili iko  shamba, Jussa anawashwa na nini  mitaani?

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC  Zanzibar, Idara  ya Itikadi , Uenezi na Mafunzo,  Khamis  Mbeto  Khamis, ameeleza hayo na kumtaka  Jussa ajiandae  kushuhudia matokeo  yatokanayo na nguvu  ya umma ifikapo  oktoba Mwaka huu.

Mbeto  alimtaka Jussa  kuacha propaganda zilizopitwa  na wakati huku akidhani atamudu kuwagawa wana CCM kwa  porojo zake,  uzushi na ufataani  wake, badala yake ametakiwa ajue kuwa muda  umekwisha na sasa atashuhudia   maamuzi ya haki yakipita. 

Alisema utendaji wa SMZ  uliotokana na ubora wa  Sera,  Mipango na mikakati   thabit ,imetoa   matokeo chanya,  yenye   tija na ufanisi  , na sasa  hiyo ndio tiketi  itakayomrudisha  madarakani  Rais wa Zanzibar  Dk Mwinyi .

"Kila mcheza kwao hutunzwa, kwa Maendeleo  yalioletwa na Serikali ya Rais Dk Mwinyi ,wananachi wameapa kumrudisha  madarakani  ima faima . Jussa omba uhai  ukishuhudie kimbunga Hidaya ' Alisema  Mbeto

Aidha, Katibu huyo Mwenezi,  aliutaja ushindi wa CCM  hautaki  tochi, kwani  kila mwananchi  ameona kazi  iliofanywa  na Serikali  ya Mapinduzi  Zanzibar  miaka mitano  iliopita.

"Rais  Dk  Mwinyi amemaliza kazi ya kutumikia wananchi  miaka mitano  iliopita , , jukumu pekee mbele yake ni kukamilisha kazi ya miaka mitano  ijayo. Zanzibar itabadilika na kuwa  Dubai , Thailand au Hong Kong ya Afrika  Mashariki " Alieleza

Akieleza kuhusu  madai ya Jussa aliyedai kuwa Rais Dk Mwinyi ametuma wagombea majimboni, Mbeto aliwataka wana CCM  kupuuza porojo hizo  za kitoto na kusema kazi ya kupandikiza wagombea ni Jussa  na wenzake saba ndani   ACT  Wazalendo. 

Aidha, Rais  Dk Samia Suluhu  Hassan na Rais Dk  Mwinyi  walishatangaza hadharani wakiwa jijini Dodoma  hawana mgombea yeyote  aliyetumwa na viongozi  hao kwenye  jimbo lolote nchini. 

"Dk Mwinyi hajamtuma mgombea yeyote. Kila mwana CCM  aliyekwenda jimboni ameamua  kwa utashi wake .Wajumbe  ndio wenye maamuzi  yupi apitishwe kwa mujibu wa  sifa zake "Alieleza Mbeto. 

Katibu  huyo Mwenezi  aliongeza kusema  Rais Dk Mwinyi  mapema kabisa baada ya kuingia madarakani, aliikataa Siasa za majibizano na  malumbano  majukwaani, akachagua kazi ya kutumikia wananchi na kujenga  Zanzibar kimaendeleo   .

Pia Mwenezi   huyo alimtaka Jussa  aendelee na kazi ya  kuwapa matumaini hewa wafuasi  wake lakini  ukweli  wa mambo  utajulikana pale wananchi watakapopitisha maamuzi ya kidemomrasia.

Mbeto: Jussa pilipili asoila inamuwashia nini Mbeto: Jussa pilipili asoila inamuwashia nini Reviewed by Gude Media on 11:37:00 AM Rating: 5

No comments

Note: Only a member of this blog may post a comment.