Mbeto ampigia saluti Rais Dk. Samia Dira ya Taifa 2025-2050


Na Mwandishi  wetu, zanzibar

Chama Cha Mapinduzi  kimesifu  mpangilio wa malengo katika Dira ya Maendeleo  ya Taifa ya Mwaka 2025 - 2050 kwa  kuiitaja  ni  njia na ramani sahihi ya kufikia Maendeleo na jinsi  kushughulika na changamoto za msingi  katika  Taifa 

Pia imesisitiza  Dira hiyo imelenga kuiongoza Tanzania ielekee na  kuwa nchi yenye uchumi imara, jumuishi na yenye kujenga  nguvu ya ushindani.

Katibu wa kamati Maalumu ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis  Mbeto  Khamis, ameeleza hayo huku akisifu dhamira njema  ya Rais Dk Samia  Suluhu  Hassan itakayosukuma mbele   ari ya  maendeleo.

Mbeto alisema  mikakati ya kujenga jamii  yenye elimu, afya bora,  makazi salama na mazingira endelevu, ni katika  kukabiliana  na Mabadiliko ya Tabia ya nchi, huo ndio  mpango na mkakati  madhubuti.

"Dira ya Taifa ya maendeleo  ilioziduliwa na Rais Dk Samia imebeba matumaini ya Watanzania. Ni Dira iliodhamiria kufikia  mabadiliko na kuharakisha maendeleo ya kweli", alisema Mbeto. 

Ameitaja  Dira hiyo itajenga msingi wa kukuza haiba ya  utawala bora, kudumisha Amani, Usalama na Utulivu, ikiwa ni kukuza ustawi wa nguzo tatu muhimu na dhima ya  kuinua  maendeleo ya Taifa. 

"Kujenga Uchumi jumuishi na shindani  hapo mmeshajua kipi  mnachokitaka . Mkiwapatia  uwezo  watu  wenu utakaoweka msukumo wa maendeleo mmeshafanikiwa. Hata mkipanga mikakati ya kisera ya  uhifadhi   mazingira mmeshajiandaa kifikra na kisera" Alisema 

Aliongeza kusema  iii kufanikisha malengo  hayo na mengine , Dira  hiyo imezitaja sekta kipaumbele kama  kilimo, Utalii, Viwanda na Madini.

"Pia  kuna sekta ya  uchumi wa Buluu, ubunifu na michezo, pamoja na huduma za kifedha  zote zimetajwa kwa lengo la kuharakisha mabadiliko na kasi ya maendeleo  " Alieleza

Pia Katibu  Mwenezi  huyo,  alisifu Dira hiyo  ya taifa  kwa kuweka vichocheo muhimu kama  usafirishaji fungamanishi, Nishati, Teknolojia, Utafiti na mageuzi ya kidijitali yatayochochea shime ya maendeleo kwa haraka.

"CCM kwetu sisi  ni fahari kuwa na Dira ya Taifa makini  hadi  2050 itaongozwa na Mpango wa Maendeleo wa Miaka 25. Kilichobaki  ni usimamizi makini  na utekelezaji  mzima wa mipango ya pamoja" Alisema Katibu Mwenezi  huyo